Wednesday, May 7, 2014

MANENO YA KWELI YASIYO NA CHEMBE YA SHAKA NDANI YAKE


Uislamu kamwe haujawahi kuwa na uadui dhidi ya Ukristo. Bali, tangu mwanzo wa kudhihiri kwake ulifungua milango ya majadiliano: “Na utawaona walio karibu zaidi (kwa mapenzi) na waumini ni wale wanaosema:  Sisi ni Wakristo.  Hayo ni kwa sababu wako miongoni mwao wanachuoni na wamchao Mwenyezi-Enzi-Mungu, na kwamba wao hawatakabari”  (Sura Maidah: 82)

Heshima kubwa kwa Yesu Kristo na kwa mama yake Mariam Mtakatifu ni sehemu ya kanuni za mafundisho ya Uaislam: “Na (kumbukeni) malaika waliposema:  Ewe Mariam, Hakika Mwenyezi-Enzi-Mungu amekuchagua na amekutakasa, na amekuchagua kuliko wanawake wote ulimwenguni”. (Aal Imran: 43)

Kufungua  milango ya majadiliano ni kitu kinachopewa  umuhimu mkubwa katika Uislam, kwa sababu kwa upande mmoja mazungumzo na majadiliano haya hufanywa kwa ustahamilivu na utulivu na kwa upande mwingine ni kitu cha kimataifa “Sema: Enyi watu wa kitabu, njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, tusimwabudu ila Mwenye-Enzi-Mungu tu, wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni waungu badala       ya Mwenye-Enzi-Mungu.  Basi wakikataa, waambieni:  Shuhudieni kwamba sisi ni wenye kunyenyekea (kwa Mwenye-Enzi-Mungu) (Aal Imran: 64)

Kama Wakristo wasingekuwa na chuki wangefanya juhudi makhsusi na ya makusudi ya kuichapisha Qur’an pembezoni mwa Injili zao. badala ya Torati ya Agano la Kale ambalo halikumtaja Kristo wala mama yake hata mara moja.  Theluthi nzima ya Qur’an inaelezea maisha ya Kristo na mamaye Mariam.  Hivyo wangelifahamu mengi ndani ya Qur’an kwani imejitosheleza kwa hilo.

Kuna sura nzima ya Qur’an iliyopewa jina la  familia ya Kristo:Al Imran (familia ya Imran). Neno “Al” hupewa familia maalumu zenye hadhi,utukufu na daraja ya juu.   



Aidha, katika Qur’an Tukufu kuna sura nyingi sana zinazoelezea masuala ya Yesu ‘Masih’.  Jinsi gani alivyokuwa akifikisha ujumbe aliotumwa na jinsi alivyoweza kudhihirisha miujiza aliyopewa na Mola wake ili awathibitishie wafuasi wake ‘Mayahudi.  Mfano wa sura hizo ni Suratul Maidah ‘meza’, ndani ya sura hii kuna miujiza mitatu, ambayo haikutajwa katika kitabu chochote cha Injili, isipokuwa Qur’an pekee.  Nayo ni kama ifuatayo.

1.       Uteremshwaji wa chakula kutoka mbinguni: “Akasema Isa bin Mariam: 
Ewe Mwenye-Enzi-Mungu, Mola wetu, tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe dalili itokayo kwako, na turuzuku, na wewe ni mbora wa wanaouruzuku.  Mwenye-Enzi-Mungu akasema:  Bila shaka mimi nitakiteremsha juu yenu, lakini miongoni mwenu atakayekataa mafundisho yangu baada ya haya, basi mimi nitamuadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yeyote katika walimwengu” 

2.       Kuwapa ndege uhai: “….. na ulipotengeneza udongo sura ya ndege
ukampulizia akawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu” 

3.       Kuzungumza na watu katika utoto: “(kumbuka) Mwenye-Enzi-Mungu
atakaposema:  Ewe Isa bin Mariam; kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa roho mtakatifu, ukazungumza na watu katika utoto na katika utu uzima wako”.

Kuna sura ndani ya Qur’an iliyopewa jina la Mariam, mama wa Kristo:  Na mtaje Mariam kitabuni alipojitenga na jamaa zake, (akaenda) mahala upande wa mashariki.  Na akaweka pazia kujikinga nao, kisha tukampeleka malaika wetu aliyejimithithilisha kwake kama mtu kamili.  (Mariam) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ikiwa unamuogopa Mwenye-Enzi-Mungu, (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako, nimetumwa ili nikubashirie kupata mtoto mtakatifu.  Akasema: Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanaume yeyote wala mimi si asherati?  (Malaika) akasema:  Ni kama hivyo, Mola wako amesema; haya ni rahisi kwangu, na ili tuufanye muujiza kwa watu na rehma itokayo kwetu, na ni jambo ambalo limekwisha hukumiwa litokee

Vile vile kuna sura nyingine iliyopewa jina la watu wa pangoni: Alkahf: “Hakika wao ni vijana waliomwamini Mola wao, nasi tukawazidisha katika muongozo


Hizi sura tatu, Al-Maidah, Mariam na Alkahf, ni miongoni mwa sura ndefu katika Qur’an............................................ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment