Friday, May 9, 2014

MANENO YA KWELI YASIYO NA CHEMBE YA SHAKA NDANI YAKE - 2



 ..........Hata hivyo, pamoja na hayo yote, Mustashriqiina (orientists) na wamishionari wanaunyima Uislam na Mtume wake kila aina ya sifa bora na hawana imani nayo.  Wanataka kuwambia Wakristo kabla ya kuudurusu na kuustaajabia Uislam ambao ni dini na ustaarabu katika historia, kwamba Uislam ni mchanganyiko usio lingana wala kuafikiana na  Uyahudi, Ukristo na Upagani.  Tatizo walilo nalo ni ujinga mkubwa au ushabiki wa upofu uliopindukia, chuki na inda kubwa au yote kwa pamoja.  Ukosefu wa mtazamo sahihi umewapelekea kufika kwenye hitimisho potofu katika uhakiki na utafiti wao.

Huwezi kukosa kuona kitu hata kimoja kinachoaminiwa na dini zote tatu. Ni ajabu kutokuta itikadi moja iliyonadiwa na mitume wote, ijapokuwa dini zipo nyingi.  Nabii Mussa (A.S) alikuja baada ya Ibrahim (A.S) na Mussa (A.S) aliyaamini mafundisho aliyokuja nayo Ibrahim; Issa (A.S) ‘Yesu’ vilevile aliyekuja baada ya hao wote aliyaamini mafundisho yao kuwa ni ya kweli, na hatimaye  Muhammad (S.A.W) ambaye ndiye wa mwisho kabisa, naye amefuata njia hiyo hiyo ya kuyaamini mafundisho ya mitume waliofangulia.  
Rejea (Sura 2:285) (2:130) (2:285)

“Mtume (S.A.W) ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waislam wote wamemwamini Mwenye-Enzi-Mungu (S.W), na malaika wake na vitabu vyake, na mitume yake ‘yote’ wanasema “Hatutofautishi baina ya yeyote katika mitume yake.  Na husema tumesikia na tumetii …”

Uislam haujasomwa kikamilifu katika vyuo vikuu vingi vya Kimagharibi.  Nasikitika kusema kuwa huenda jambo hili lilifanywa kwa madhumuni maalum; hata hivyo kumekuwepo na baadhi ya waliokwenda kinyume na mtazamo na mwelekeo huo:  Wasomi kadhaa wa kimataifa hawakuwa na itikadi za upendeleo.  Wasomi hao ni kama vile Carlyle, Tolstory, Lord headley, Bernard Shaw, Edward Gibbon, Etienne Dinet, Count Henry de Castry, Renet Ginout, Dr. Griniet, na Roger Garody.  Ni jambo zuri mno kama Wamagharibi wataachana na chuki za kimapokeo dhidi ya Uislam ambazo zimekuwa zikiongezwa bila ya ukweli wowote na mabeberu wa kisiasa na viongozi wao wa kidini wenye ushabiki na inda nyoyoni mwao, na badala yake wausome na kuudurusu Uislam bila upendeleo wowote kama walivyofanya watu waliotajwa hapo juu.  Uongo na uzushi wa mustashriqiina na wamishionari hujirudia mwanzoni mwa kila kizazi.  Hawajapata mambo mapya kwa karne nyingi sasa.  Hung’ang’ania kuzusha mambo yafuatayo bila uthibitisho:-

-              Muhammad hakuwa Mtume kwa sababu alijifunza Qur’an au aliipokea kutoka kwa mtawa aliyeitwa Bahira au kutoka kwa Waraqah bin Nawfal.  {16:105}

“Wanaozua uwongo kwa kusema kuwa Muhammad amefundishwa Qur’an na huyo ‘Mrumi’ ni wale wasio ziamini aya za Mwenye-Enzi-Mungu na hao ndio waongo”

-              Uislam ulienezwa kwa nguvu ya upanga:  Watu walilazimishwa kuingia katika Uislam la sivyo wauawe, wakati ambapo Wahubiri wa Kikristo walipata wafuasi wengi kwa kutumia huruma na ukweli.

-              Uislam uliwakandamiza wanawake na kutangaza ndoa ya mitala.

Kashfa nyingi zilizotolewa na mustashriqiina na wamishionari ni upotoshaji mkubwa.  Ni vizuri wakafuata njia ya utafiti wa kisayansi unaowataka wasomi waadilifu na makini kuusoma Uislam katika namna ambayo Waislam huitumia kuusoma, yaani kuepukana na chuki za kupangwa, kuondokana na madhumuni yasiyokuwa ya kisayansi au mawazo ya ajabu ajabu yasiyotabirika ambayo hupotosha na kutoa mahitimisho yaliyoandaliwa na hivyo kuwa mbali na ukweli.

Mbali na hilo, uzushi huu unaowadhihaki Waislam, unaweza kukanushwa kirahisi kwa ushahidi na uthibitisho.  Wale wanaoushutumu Uislam tunawakumbusha aibu na mapungufu yao wenyewe kwamba, mkutano wa Nicea uliofanyika mwaka 325 A.D.  uliamuru kuchomwa moto kwa vitabu vyote visivyoafikiana na mafundisho ya Kanisa na kupiga marufuku kila kitu kilicho kinyume na imani za Kanisa.  Kwa njia hii Kanisa linajaribu kudhibiti nyoyo na kuzizuia roho za watu ambao zililazimishwa kuamini kile tu kilichoafikiwa katika mkutano huo.

Mkutano huo wa wakuu wa Kanisa ulifanya dhuluma kwa kuweka marufuku hiyo na ulifanya dhambi kwa uchomaji wa vitabu vya dini.  Vikao vilivyofuata baadaye vilirekebisha matendo hayo ya kijinga na kuondosha marufuku iliyowekwa juu ya vitabu vilivyo na elimu sawa ya dini.

Wanahistoria wa Kikristo wanasema kuwa kulikuwepo na Injili nyingi.  Lakini mwishoni mwa karne ya 2 na mwanzoni mwa karne ya tatu kanisa liliamua kubaki na Injili ambazo liliamini kuwa zilikuwa sahihi na hivyo likachagua Injili nne zilizopo leo hii na kuwalazimisha Wakristo kuzifuata sambamba na kuweka udhibiti na ukaguzi mkali na wa hali ya juu ili kuzifuta kabisa zile Injili nyingine.  Je watu wa Ulaya wamewahi kujali au kujiuliza kwamba Injili zilizofutwa zilikuwa na nini na kwa nini zilipigwa marufuku na nani aliyekuwa na haki ya kuzifuata?  Hata hivyo pamoja na kufanya marekebisho na kuvibakisha vitabu walivyoamini kuwa vilikuwa na mafundisho mazuri, Injili hizo sasa zimeingizwa mikono ya watu na kuufanya ukweli wa mafundisho yake kuwa wa kutia shaka kubwa, isipokuwa Injili aliyoiacha Yesu tu.


Wanaushaumbulia Uisilam kwamba ulienea kwa nguvu ya upanga!  Kuna tofauti kubwa sana kati ya harakati ufunguzi iliyostaarabika ya kueneza mafundisho, na kulazimisha mafundisho na imani kwa njia ya upanga, kama Charlemagne alivyofanya katika zama za kati, na kama wamishionari waliosuhubiana na utafiti wa kijografia katika zama za leo, walivyofanya huko Afrika na Amerika. (wamishionari hao) waliwaangamiza watu wote, waliingia katika biashara ya utumwa na kuwachukua mamia kwa maelefu ya watu hao kama mateka na kupora maliasili za maeneo husika.  Yote hayo yakifanywa kwa jina la Yesu na kwa baraka za Papa.  Lakini Uislam ulitoa fursa huru kwa mwenye kuamua kuyafuata mafundisho yake ayafuate.

 
KITABU PEKEE AMBACHO HAKIJAWAHIWA NA HAITOTOKEA KUHARIRIWA WALA KUTOLEWA TOLEO JIPYA
Qur’an Tukufu inasema:- ...........................................................ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment