Thursday, August 30, 2012

FAHAMU KUHUSU UISILAMU NA UKIRISTO

 KATI YA MIONGOZO YA DINI TOFAUTI NI MUONGOZO UPI UMEMTAJA YESU IPASAVYO, MAMA YAKE YESU NA FAMILIA YA YESU?
Uislamu kamwe haujawahi kuwa na uadui dhidi ya Ukristo. Bali, tangu mwanzo wa kudhihiri kwake ulifungua milango ya majadiliano: “Na utawaona walio karibu zaidi (kwa mapenzi) na waumini ni wale wanaosema:  Sisi ni Wakristo.  Hayo ni kwa sababu wako miongoni mwao wanachuoni na wamchao Mwenyezi-Enzi-Mungu, na kwamba wao hawatakabari” (5:82).

Heshima kubwa kwa Yesu Kristo na kwa mama yake Mariam Mtakatifu ni sehemu ya kanuni za mafundisho ya Uaislam: “Na (kumbukeni) malaika waliposema:  Ewe Mariam, Hakika Mwenyezi-Enzi-Mungu amekuchagua na amekutakasa, na amekuchagua kuliko wanawake wate ulimwenguni”.(3:43)

Kufungua  milango ya majadiliano ni kitu kinachopewa  umuhimu mkubwa katika Uislam, kwa sababu kwa upande mmoja mazungumzo na majadiliano haya hufanywa kwa ustahamilivu na utulivu na kwa upande mwingine ni kitu cha kimataifa “Sema: Enyi watu wa kitabu, njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, tusimwabudu ila Mwenye-Enzi-Mungu tu, wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni waungu badala       ya Mwenye-Enzi-Mungu.  Basi wakikataa, waambieni:  Shuhudieni kwamba sisi ni wenye kunyenyekea (kwa Mwenye-Enzi-Mungu)(3:64)

Kama Wakristo wasingekuwa na chuki wangefanya juhudi makhsusi na ya makusudi ya kuichapisha Qur’an pembezoni mwa Injili zao. badala ya Torati ya Agano la Kale ambalo halikumtaja Kristo wala mama yake hata mara moja.  Theluthi nzima ya Qur’an inaelezea maisha ya Kristo na mamaye Mariam.  Hivyo wangelifahamu mengi ndani ya Qur’an kwani imejitosheleza kwa hilo.

Kuna sura nzima ya Qur’an iliyopewa jina la  familia ya Kristo:Al Imran (familia ya Imran). Neno “Al” hupewa familia maalumu zenye hadhi,utukufu na daraja ya juu.  

Aidha, katika Qur’an Tukufu kuna sura nyingi sana zinazoelezea masuala ya Yesu ‘Masih’.  Jinsi gani alivyokuwa akifikisha ujumbe aliotumwa na jinsi alivyoweza kudhihirisha miujiza aliyopewa na Mola wake ili awathibitishie wafuasi wake ‘Mayahudi.  Mfano wa sura hizo ni Suratul Maidah ‘meza’, ndani ya sura hii kuna miujiza mitatu, ambayo haikutajwa katika kitabu chochote cha Injili, isipokuwa Qur’an pekee.  Nayo ni kama ifuatayo.


1.       Uteremshwaji wa chakula kutoka mbinguni: “Akasema Isa bin Mariam: 
Ewe Mwenye-Enzi-Mungu, Mola wetu, tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe dalili itokayo kwako, na turuzuku, na wewe ni mbora wa wanaouruzuku.  Mwenye-Enzi-Mungu akasema:  Bila shaka mimi nitakiteremsha juu yenu, lakini miongoni mwenu atakayekataa mafundisho yangu baada ya haya, basi mimi nitamuadhibu adhabu ambayo sijamwadhibu yeyote katika walimwengu

2.       Kuwapa ndege uhai: “….. na ulipotengeneza udongo sura ya ndege
ukampulizia akawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu

3.       Kuzungumza na watu katika utoto: “(kumbuka) Mwenye-Enzi-Mungu
atakaposema:  Ewe Isa bin Mariam; kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa roho mtakatifu, ukazungumza na watu katika utoto na katika utu uzima wako”.

Kuna sura ndani ya Qur’an iliyopewa jina la Mariam, mama wa Kristo:  Na mtaje Mariam kitabuni alipojitenga na jamaa zake, (akaenda) mahala upande wa mashariki.  Na akaweka pazia kujikinga nao, kisha tukampeleka malaika wetu aliyejimithithilisha kwake kama mtu kamili.  (Mariam) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ikiwa unamuogopa Mwenye-Enzi-Mungu, (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako, nimetumwa ili nikubashirie kupata mtoto mtakatifu.  Akasema: Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanaume yeyote wala mimi si asherati?  (Malaika) akasema:  Ni kama hivyo, Mola wako amesema; haya ni rahisi kwangu, na ili tuufanye muujiza kwa watu na rehma itokayo kwetu, na ni jambo ambalo limekwisha hukumiwa litokee

Vile vile kuna sura nyingine iliyopewa jina la watu wa pangoni: Alkahf: “Hakika wao ni vijana waliomwamini Mola wao, nasi tukawazidisha katika muongozo

Hizi sura tatu, Al-Maidah, Mariam na Alkahf, ni miongoni mwa sura ndefu katika Qur’an.

 Hata hivyo, pamoja na hayo yote, Mustashriqiina (orientists) na wamishionari wanaunyima Uislam na Mtume wake kila aina ya sifa bora na hawana imani nayo.  Wanataka kuwambia Wakristo kabla ya kuudurusu na kuustaajabia Uislam ambao ni dini na ustaarabu katika historia, kwamba Uislam ni mchanganyiko usio lingana wala kuafikiana na  Uyahudi, Ukristo na Upagani.  Tatizo walilo nalo ni ujinga mkubwa au ushabiki wa upofu uliopindukia, chuki na inda kubwa au yote kwa pamoja.  Ukosefu wa mtazamo sahihi umewapelekea kufika kwenye hitimisho potofu katika uhakiki na utafiti wao.

Huwezi kukosa kuona kitu hata kimoja kinachoaminiwa na dini zote tatu. Ni ajabu kutokuta itikadi moja iliyonadiwa na mitume wote, ijapokuwa dini zipo nyingi.  Nabii Mussa (A.S) alikuja baada ya Ibrahim (A.S) na Mussa (A.S) aliyaamini mafundisho aliyokuja nayo Ibrahim; Issa (A.S) ‘Yesu’ vilevile aliyekuja baada ya hao wote aliyaamini mafundisho yao kuwa ni ya kweli, na hatimaye  Muhammad (S.A.W) ambaye ndiye wa mwisho kabisa, naye amefuata njia hiyo hiyo ya kuyaamini mafundisho ya mitume waliofangulia. Rejea (Sura 2:285) (2:130) (2:285)

“Mtume (S.A.W) ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waislam wote wamemwamini Mwenye-Enzi-Mungu (S.W), na malaika wake na vitabu vyake, na mitume yake ‘yote’ wanasema “Hatutofautishi baina ya yeyote katika mitume yake.  Na husema tumesikia na tumetii …”

Uislam haujasomwa kikamilifu katika vyuo vikuu vingi vya Kimagharibi.  Nasikitika kusema kuwa huenda jambo hili lilifanywa kwa madhumuni maalum; hata hivyo kumekuwepo na baadhi ya waliokwenda kinyume na mtazamo na mwelekeo huo:  Wasomi kadhaa wa kimataifa hawakuwa na itikadi za upendeleo.  Wasomi hao ni kama vile Carlyle, Tolstory, Lord headley, Bernard Shaw, Edward Gibbon, Etienne Dinet, Count Henry de Castry, Renet Ginout, Dr. Griniet, na Roger Garody.  Ni jambo zuri mno kama Wamagharibi wataachana na chuki za kimapokeo dhidi ya Uislam ambazo zimekuwa zikiongezwa bila ya ukweli wowote na mabeberu wa kisiasa na viongozi wao wa kidini wenye ushabiki na inda nyoyoni mwao, na badala yake wausome na kuudurusu Uislam bila upendeleo wowote kama walivyofanya watu waliotajwa hapo juu.  Uongo na uzushi wa mustashriqiina na wamishionari hujirudia mwanzoni mwa kila kizazi.  Hawajapata mambo mapya kwa karne nyingi sasa.  Hung’ang’ania kuzusha mambo yafuatayo bila uthibitisho:-

-              Muhammad hakuwa Mtume kwa sababu alijifunza Qur’an au aliipokea kutoka kwa mtawa aliyeitwa Bahira au kutoka kwa Waraqah bin Nawfal.  {16:105}

“Wanaozua uwongo kwa kusema kuwa Muhammad amefundishwa Qur’an na huyo ‘Mrumi’ ni wale wasio ziamini aya za Mwenye-Enzi-Mungu na hao ndio waongo”

-              Uislam ulienezwa kwa nguvu ya upanga:  Watu walilazimishwa kuingia katika Uislam la sivyo wauawe, wakati ambapo Wahubiri wa Kikristo walipata wafuasi wengi kwa kutumia huruma na ukweli.

-              Uislam uliwakandamiza wanawake na kutangaza ndoa ya mitala.

Kashfa nyingi zilizotolewa na mustashriqiina na wamishionari ni upotoshaji mkubwa.  Ni vizuri wakafuata njia ya utafiti wa kisayansi unaowataka wasomi waadilifu na makini kuusoma Uislam katika namna ambayo Waislam huitumia kuusoma, yaani kuepukana na chuki za kupangwa, kuondokana na madhumuni yasiyokuwa ya kisayansi au mawazo ya ajabu ajabu yasiyotabirika ambayo hupotosha na kutoa mahitimisho yaliyoandaliwa na hivyo kuwa mbali na ukweli.

Mbali na hilo, uzushi huu unaowadhihaki Waislam, unaweza kukanushwa kirahisi kwa ushahidi na uthibitisho.  Wale wanaoushutumu Uislam tunawakumbusha aibu na mapungufu yao wenyewe kwamba, mkutano wa Nicea uliofanyika mwaka 325 A.D.  uliamuru kuchomwa moto kwa vitabu vyote visivyoafikiana na mafundisho ya Kanisa na kupiga marufuku kila kitu kilicho kinyume na imani za Kanisa.  Kwa njia hii Kanisa linajaribu kudhibiti nyoyo na kuzizuia roho za watu ambao zililazimishwa kuamini kile tu kilichoafikiwa katika mkutano huo.

Mkutano huo wa wakuu wa Kanisa ulifanya dhuluma kwa kuweka marufuku hiyo na ulifanya dhambi kwa uchomaji wa vitabu vya dini.  Vikao vilivyofuata baadaye vilirekebisha matendo hayo ya kijinga na kuondosha marufuku iliyowekwa juu ya vitabu vilivyo na elimu sawa ya dini.

Wanahistoria wa Kikristo wanasema kuwa kulikuwepo na Injili nyingi.  Lakini mwishoni mwa karne ya 2 na mwanzoni mwa karne ya tatu kanisa liliamua kubaki na Injili ambazo liliamini kuwa zilikuwa sahihi na hivyo likachagua Injili nne zilizopo leo hii na kuwalazimisha Wakristo kuzifuata sambamba na kuweka udhibiti na ukaguzi mkali na wa hali ya juu ili kuzifuta kabisa zile Injili nyingine.  Je watu wa Ulaya wamewahi kujali au kujiuliza kwamba Injili zilizofutwa zilikuwa na nini na kwa nini zilipigwa marufuku na nani aliyekuwa na haki ya kuzifuata?  Hata hivyo pamoja na kufanya marekebisho na kuvibakisha vitabu walivyoamini kuwa vilikuwa na mafundisho mazuri, Injili hizo sasa zimeingizwa mikono ya watu na kuufanya ukweli wa mafundisho yake kuwa wa kutia shaka kubwa, isipokuwa Injili aliyoiacha Yesu tu.

Wanaushaumbulia Usilam kwamba ulienea kwa nguvu ya upanga!  Kuna tofauti kubwa sana kati ya harakati ufunguzi iliyostaarabika ya kueneza mafundisho, na kulazimisha mafundisho na imani kwa njia ya upanga, kama Charlemagne alivyofanya katika zama za kati, na kama wamishionari waliosuhubiana na utafiti wa kijografia katika zama za leo, walivyofanya huko Afrika na Amerika. (wamishionari hao) waliwaangamiza watu wote, waliingia katika biashara ya utumwa na kuwachukua mamia kwa maelefu ya watu hao kama mateka na kupora maliasili za maeneo husika.  Yote hayo yakifanywa kwa jina la Yesu na kwa baraka za Papa.  Lakini Uislam ulitoa fursa huru kwa mwenye kuamua kuyafuata mafundisho yake ayafuate.

Qur’an Tukufu inasema:- 

          “Hakuna kulazimishwa katika dini (kuingia katika dini), hakika
uongofu umekwisha pambanuka na upotovu umedhihirishwa”

“Na sema huu ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi
anayependa akubali, na anayependa basi  akatae, kwa hakika
tumewaandalia madhalimu moto ambao kuta zake zitawazunguka”

“Lakini wakikataa, basi hakika juu yako ni kufikisha tu ujumbe uliowazi”

Injili ya Mathayo 10:34 inasema:-

          Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja
kuleta amani, basi upanga”

Bado wanadai kwamba Uislam ni dini ya upanga lakin Ukristo ni dini ya upendo, iwezekanaje? Kutokana na ushahidi wa {10:34} Mathayo?

Kanisa liliposhusha jina la mwanamke na kumdhalilisha kwa kumuona kuwa ndiye chanzo cha uovu na dhambi, Uislam ulikuja na kuinyanyua daraja ya mwanamke na kuiweka juu.  Muhammad (S.A.W) akasema:-
“Wanawake ni sawa na wanaume”. 

Uislam umemfanya mwanamke kuwa ‘Mnara’ wa wema na huruma; taji linalopamba kichwa cha kila mwanamke wa Kiislam ni mapendo na huruma.  Ndoa ya wake wingi ilienea sana na ikakubalika kwa watu wote hata watumishi wa Kanisa wenyewe.  Mtawala wa Kirumi Jastinian - mtunga sheria wa kipagani- ndiye aliyekuwa wa kwanza kufikiri juu ya kuweka sheria ya kuweka kikomo cha idadi ya wake na kuwa mmoja lakini Kanisa lilipinga fikra yake hiyo.

Uislam ulipokuja ulijaribu kuiwekea udhibiti ndoa ya wake wengi.  Ilikuwa ni kazi ngumu kuzuia mtazamo wao huu.  Bali Uislam ukaingiza utaratibu wa mwanaume mmoja kuruhusiwa kuoa wake hadi wanne.  Hii ilikuwa kama ponyo kwa watu wasiendeleze uchafu wa uzinzi.  Hakuna dhambi kwa asiyeweza kuitekeleza na wala haivunji sheria  za Uislam, ijapokuwa ni bora sana kwa wenye kuweza ‘kufanya uadilifu’ kuna faida nyingi sana katika hili kwa pande zote mbili ‘mke na mume’

          “Ndoa ya mitala ni tiba na sio matendo ya mazoea”

Nani anayesema kuwa Wamagharibi wamefungwa kuwa na mke mmoja tu?  Je siku hizi hakuna ndoa za mitala katika nchi za Kikristo?

Kwa  hakika ndoa ni mkataba unaowekwa baina ya mwanaume na mwanamke.  Lakini kwa kuwa yana husika kwa kiasi kikubwa na mustakbali wa vizazi na kwa kuwa yanaungana sana na uthabiti wa kweli wa nasaba za wahenga kupitia ndoa, Uislam unachukulia muungano huu kuwa ni kitu kitukufu.  Kama tukiiangalia ndoa kama ndoa tunakuta kuwa Wakristo huko Magharibi wana mahusiano ya kimapenzi  na wanawake wengi kuliko hata Waislam. Kwa kweli Wakristo huwa na wanawake wengi bila haya, kile anachokifanya Mwislam kwa kikomo kilichothibitishwa na madhumuni yaliyohalalishwa huchukuliwa kuwa ni aibu au kosa na kuitwa mitala, wakati ambapo Mkristo hufanya ufedhuli bila kuona haya na bila kizuizi haadhibiwi na sheria; ni uzinzi.

Maadui wa Uislam wanatambua vyema kuwa lau wangetumia sehemu ya juhudi zao katika kukashifu na kusingizia mafundisho yoyote kinyume na Uislam mafundisho hayo yangekanushwa.  Lakini ni jambo la kawaida kwamba Uislam husimama imara, kwa utukufu, hupanda milima na hatimaye kushinda  vita vyote vinavyoanzishwa na kupigana dhidi yake.  Kwamba Uislam ni dini ambayo siku zote inakwenda mbele na kukuendelea kwa rehma, ulinzi na msaada wa Allah:-

          Hakika sisi tumeiteremsha Qur’an, na hakika sisi ndio wenye
kuilinda”

Ndani ya kitabu hiki tujadili juu ya imani na mafundisho ya Uislam, si matendo yenye makosa ya baadhi ya wanaofuata dini hii kwa jina tu.  Maisha na matendo ya kweli ya baadhi ya Waislam wa siku hizi yanatofautiana na mtazamo wa Uislam wa kweli.  Uislam sio yale wayaonayo Wamagharibi katika matendo ya mtalii wa Kiarabu ambayo hukanyaga maadili yote wakati akikimbia kwa kutwetatweta kwenda kuridhisha matamanio yake, kwani sio kila Mwarabu ni Muislam na hivyo mitazamo wanayotumia kuhukumu Uislam wanakosea.

Katika kurasa zijazo tutaweka mahakama.  Katika kila kesi au kikao cha mahakama Uislam utaitwa kusimama kama mshitakiwa, mwendesha mashtaka ataleta mashtaka dhidi ya Uislam.  Huyu mwendesha mashtaka atakuwa ni mustashriqiina au mmishionari.  Tutataja jina la kitabu chake ambacho ndani yake tuhuma zimetokea.  Hakimu atauita Uislam kuja kujitetea.  Huyu hakimu ni akili yenye busara,
yenye umakini na hekima inayopenda kudhihirisha ukweli, ikaacha upendeleo na ambayo haina ushabiki.

Uislam utasimama kutii amri ya hakimu na hautahitaji mwanasheria kuutetea kwani kesi iko wazi na dhahiri na Uislam unajiamini utasoma na kutoa hoja zake kwa sauti kupinga mashtaka.  Utetezi wake utaandikwa na ushahidi wake utadokezewa kwa uwazi katika vitabu rejea ili wale wanaohudhuria mahakamani waweze kupata ushahidi huo kwa urahisi.  Kesi itahitimishwa na hakimu ambaye, hatatoa hukumu ya kuachiwa huru au kutiwa hatiani, kwani wasomaji au wasikilizaji wana tabia tofauti za akili na kufikiri.  Sitataja hukumu ya kila mshtaka kulazimisha mtazamo wangu ambao, nina hakika kwamba Uislam hauna dosari na hauna hatia ya mashtaka ya mustashriqiina na wamishionari.  Ni ukamilifu na hauna dosari yoyote, na hauna kasoro zozote, lakini nataka msomaji agundue jambo hili yeye mwenye.

Mwisho ninapenda kuwatanabahisha wale ambao wamejiamulia kashfa dhidi ya Uislam kama kazi yao na kujitolea kuuvunjia heshima, kwamba ukweli na nguvu na ni wenye kushinda na kwamba hisia za chuki katika maamuzi siku zote humpeleka mtu kwenye hitimisho lenye makosa.

Vile vile tunawakumbusha kuwa shutuma zao na mazungumzo yao ya bure yanafahamika vyema na hurudiwarudiwa mara kwa mara, na kwamba Uislam unapotoshwa katika akili zao si katika uhalisia wake.

“Hakika  Mwenye-Enzi-Mungu amewafanyia hisani kubwa Waislam alivyowaletea Mtume miongoni mwao, anayewasomesha aya zake.  Aya zake na anawatakasa na kuwafundisha kitabu na hekima na bila shaka kabla ya hapo walikuwa katika upofu mkubwa” {3:164}

Ninapenda kuwaambia wasomaji kuwa mazungumzo au majadiliano yapo wazi kwa watu wote, kwa utulivu, bila wasiwasi, kwa uadilifu, bila upendeleo, bila chuki, uongo na fujo ambazo kamwe hazipelekei kwenye matokeo yoyote mazuri.

Basi majadiliano baina ya ustaarabu masuala mbali mbali na yaanze katika ulimwengu huu ambapo masafa na na umbali umeondoshwa kuonyesha ukweli.  Mtu anaweza kuwa Damascus, muda wa asubuhi na jioni akawa London au New York, au jioni anaweza kutembelea Paris au Rome na asubuhi akazuru Karatch au Tokyo.  Majadiliano ni njia nzuri ya kudhihirisha ukweli.

Zama mpya au mwanzo wa historia mpya baada ya kufunga mlango wa karne ya ishirini zinapaswa kuanza kwa mtu kutafuta mambo mema popote yalipo hata kama yamo katika Uislam ambao ushabiki wa Kanisa umeiharibu sura yake kwa makusudi machoni mwa Wamagharibi ili kuwazuia wasiukaribie.

Ni wakati mwafaka kwa wapenda elimu na ukweli, kwa kutumia majadiliano ya busara na maarifa, waondokane na picha ya uongo ya Uislam iliyochorwa na ushabiki wenye chuki wa wabebaji wa msalaba.  Uzayuni una nafasi kubwa katika kutangaza propaganda hizo kwa kutumia uwezo wa kila aina ya vyombo vya habari inavyorimiliki.

Katika maisha ya kila siku mtu hufanya juhudi kujua iwapo habari alizosikia ni za kweli au sio za kweli.  Huwenda likawa tukio la kawaida linalorudiwarudiwa mahali popote ulimwenguni.  Katika kutafuta ukweli wa habari au ripoti aliyoisikia binadamu hujiheshimu yeye na huiheshimu akili yake, basi itakuwaje iwapo ukweli anaoutafuta unahusu dini yeye mabilioni ya wafuasi au waumini.  Je hapaswi kuiandaa akili yake katika kutaka kujua misingi na mafundisho ya kweli? Je wakati haujafika wa kuudurusu Uislam kwa busara na bila ya ushabiki na upendeleo katika namna ile ile inayofanywa na mtu mwenye akili kudurusu jambo lolote popote pale ulimwenguni katika maisha yake ya kila siku?  Ninatambua kuwa jibu sahihi la mtu makini ni ndiyo.

No comments:

Post a Comment