Wednesday, April 2, 2014

BARUA YA MTUME MUHAMMAD[S.A.W] KWA MFALME WA WARUMI

BARUA YA MTUME MUHAMMAD[S.A.W] KWA MFALME WA WARUMI:
-------------------------------------------------------------------------------
Abdullah bin Abbas,anasimulia kwamba Mtume wa Allah[S.A.W] alimuandikia[barua] Heraclius[Mfalme wa warumi[Byzantines] (610–641)]na kumualika katika uislamu,hivyo alimpa barua sahaba wake anayeitwa Dihya al-Kalbi. Dihya alimkabidhi gavana wa Busra ambaye aliituma kwa Heraclius.
Heraclius,kama alama ya kumshukuru Mwenyezi Mungu,alitembea kutoka Hims mpaka Ilya (i.e. Jerusalem) wakati Mwenyezi Mungu alipompa ushindi dhidi ya kikosi cha Persian.Wakati barua ya Mtume wa Allah[S.A.W] ilipomfikia Heraclius,alisema baada ya kuisoma,"Nitafutieni yeyote katika watu wake[waarabu wa kabila la Quraish] kama yupo hapa,ili nimuulize kuhusu Mtume wa Allah[S.A.W]!".Wakati huo Abu Sufyan bin Harb alikuwa Shaam[ nchi za Syria, Lebanon, Palestina, na Jordan] akiwa pamoja na watu wa kabila la Quraish ambao walikuja kama wafanyabiashara baada ya kuwafikiana mkataba wa amani baina ya Mtume wa Allah[S.A.W] na wapagani wa kiqureishi.
Abu Sufyan alisema,"Mjumbe wa Heraclius alituona sisi katika baadhi ya maeneo ya Shaam,hivyo anakanichukua mimi na wenzangu kwenda Ilya na tukakaribishwa alipokuwepo Heraclius.Tulimuona amekaa katika mahakama yake tukufu huku amevaa kofia ya kifalme,amezunguukwa na wazee watukufu wa kirumi.Akamwambia mfasiri[translator] wake, "Waulize ni nani kati yao ana uhusiano na mtu anayedai kwamba ni Mtume"
Abu Sufyan aliongezea,"Nilijibu,mimi ndie jamaa wa karibu zaidi kwake,".Alimuuuliza"Una ujamaa wa karibu kiasi gani na yeye " .Nikajibu,"Yeye ni mjomba wangu[cousin],na hakuna mwengine kutoka katika kabila la Abd Manaf katika msafara[huu] isipokuwa mimi".Heraclius akasema,"Mleteni karibu".Kisha aliwaamrisha wenzangu wakae nyuma yangu karibu na mabega yangu na akamwambia mfasiri wake,"Waambie wenzake kwamba nitamuuliza mtu huyu kuhusu mtu anayedai kuwa ni mtume.Akisema uongo,basi wampinge haraka"
Abu Sufyan aliongezea,"Wallahi, isingelikuwa ni aibu kwamba wenzangu wataniita muongo,nisingelizungumza ukweli kumhusu yeye[mtume] wakati aliponiuliza.Lakini nililichukulia hilo ni aibu kuitwa muongo na wenzangu,hivyo nilizungumza ukweli".
Kisha alimuambia mfasiri wake,"ni aina gani ya familia anatokea "Nikajibu, "anatokea katika familia tukufu kati yetu"Akasema,"Kuna yeyote miongoni mwenu aliyedai hivyo[utume] kabla?"Nikasema,"Hapana"."Kuna yeyote aliyewahi kumlaumu kwa kusema uongo kabla hajadai alichokidai[utume]?".Nikasema,"Hapana"."Kuna yeyote katika mababu zake alikuwa mfalme?".Nikajibu,"Hapana".Akasema,"ni watukufu[matajiri] au mafukara/masikini wanaomfuata".Nikajibu,"Ni masikini ndio wanaomfuata".Akasema,"Je, wanaengezeka au wanapungua[kila siku ] ?" Nikajibu, " Wanaongezeka".
Kuna yeyote kati ya wanaoikubali[wanaosilimu] dini yake na akawa haridhii na kisha kuachana na dini yake?".Nikasema,"Hapana".Akasema,"Je anavunja ahadi zake".Nikajibu,"hapana,lakini sasa hivi tupo katika mkataba wa amani na yeye,na tunaogopea anaweza akatusaliti"Abu Sufyan akaongezea,"Ukiachana na sentensi ya mwisho,sikuweza kusema chochote dhidi yake"
Heraclius kisha akauliza,"Je,mushawahi kupigana vita na yeye? "Nikajibu, "Ndio ". Akasema,"ni yapi matokeo ya vita vyenu na yeye"Nikajibu,"Baadhi ya wakati anaibuka mshindi,na baadhi ya wakati ni sisi".Akasema,"Nini anaamrisha mukifanye"
Nikasema,"Tumuabudu Allah pekee na tusimshirikishe na wengine pamoja nae[katika ibada] na tuache yale yote ambayo mababu zetu walikuwa wakiyaabudu .
Anatuamrisha tusimamishe swala,tutoe zakkah,tujiepushe na uchafu[uzinzi nk] ,tutekeleze ahadi na turudishe amana tulizoaminiwa"."Wakati niliposema hayo,Heraclius alimwambia mfasiri wake,"Mwambie,nimekuuliza kuhusu ukoo[familia] yake,na jibu lako lilikuwa ni kwamba ametoka katika familia tukufu,kwa hakika Mitume yote imetoka katika koo tukufu za mataifa yao.
Kisha nimekuuliza,ama yeyote kati yenu amedai kitu hicho[utume] na jibu lako lilikuwa ni 'hapana',kama jibu lingekuwa "ndio" ningefikiria kwamba mtu huyu anafuata dai ambalo limeshasemwa kabla yake.Wakati nilipokuuliza ama ameshawahi kulaumiwa kwa kusema uongo,jibu lako lilikuwa ni 'hapana'.Hivyo nimelichukulia hilo mtu ambaye hasemi uongo, basi katu hawezi kusema uongo kuhusu Mungu.
Kisha nilikuuliza ama yeyote katika mababu zake alikuwa mfalme.jibu lako lilikuwa ni 'Hapana' na kama lingekuwa 'ndio' ningefikiria kwamba mtu huyu anataka kuchukua tena ufalme wa mababu zake.Wakati nilipokuuliza,ama matajiri au masikini ndio wanaomfuata,jibu lako lilikuwa ni masikini ndio wanaomfuata.Kwa hakika hao ndio wafuasi wa Mitume.
Kisha nilikuuliza wafuasi wake wanaongezeka au kupungua,ulijibu kwamba wanaongezeka.Kwa hakika haya ni matokeo ya imani ya kweli mpaka hukamilika[katika kila kipengele].Nilikuuliza ama kuna yeyote baada ya kuingia katika dini yake anakua haridhii na kisha kuachana nayo,jibu lako lilikuwa ni 'hapana'.Kwa hakika hii ni dalili ya imani ya kweli,kwani furaha yake ikiingia na kuchanganyika na mioyo kikamilifu,hakuna atakayechukizwa nayo.
Nilikuuliza ama keshawahi kuvunja ahadi,ulijibu 'Hapana'.Na hao ndio mitume,katu hawavunji ahadi zao.Wakati nilipokuuliza kwamba unapigana na yeye na yeye anapigana na nyinyi,ulijibu ndio,na baadhi ya wakati anaibuka mshindi na baadhi ya wakati ni nyinyi.Kwa hakika hao ndio mitume,wanaingizwa katika mitihani na siku zote mwisho unakuwa ni wa kwao[wanashinda].
kisha nilikuuliza nini anawaamrisha,ukajibu kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee pasi na kumshirikisha na yeyote pamoja naye,kuacha yote ambayo mababu zenu walikuwa wakiyaabudu,kusimamisha swala,kutoa zakka,kuzungumza ukweli,kuwa wasafi[kujiepusha na uzinzi nk], kutovunja ahadi na kurudisha amana mulizoaminiwa nazo.
Hizi ni sifa za kweli za mtume,ambaye ninajua[kutoka vitabu vilivyopita] atatokea ,lakini sikujua kama atatokea miongoni mwenu.Kama unayoyasema ni kweli,basi ni muda mfupi tu ataichukua dunia chini ya miguu yangu,na kama nilijua kwamba naweza kumfikia yeye,basi hakika ningeenda haraka kukutana naye;na kama ningekuwa pamoja naye basi hakika ningeosha miguu yake".
Abu Sufyan aliongezea,"Kisha Heraclius aliulizia barua kutoka kwa mtume[S.A,W] na kisha ikasomwa.Kilichokuwemo ndani yake ni kama ifuatavyo:
"Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu;[barua hii ni] kutoka kwa Muhammad,Mja wa Allah na mtume wake,kwenda kwa Heraclius mfalme wa Byzantine[Rome].Amani iwe juu ya wafuatao uongofu. Nakualika katika uislamu[yaani kujisalimisha kwa Allah].Kubali uislamu[silimu] na utasalimika.Kubali uislamu na Mwenyezi Mungu atakupa juu yako malipo mara mbili,lakini ukiukataa mwaliko huu wa uislamu,utakuwa mwenye kuwajibika kwa kuwapotosha wafuasi wako[yaani taifa lako].
" Sema[Ewe Muhammad[S.A.W]: Enyi Watu wa Kitabu[wakiristo na mayahudi]! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu[pekee], wala tusimshirikishe na chochote[pamoja naye]; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.[3:64].
Abu Sufyan aliongezea,"Wakati Heraclius alipomaliza kauli yake,palitokea tafrani na vilio vilivyosababishwa na watukufu wa kirumi waliomzunguka yeye[Heraclius] na palikuwa na makelele mno kiasi kwamba sikuelewa walichokuwa wakikisema.Hivyo tukaamrishwa tutoke nje ya mahakama.
Wakati tulipotoka nje na wenzangu na tukawa peke yetu,niliwaambia,"Hakika, jambo la Ibn Abi Kabsha[Mtume Muhammad[S.A.W]] limepata nguvu[ na kutawala].Huyu ni mfalme wa Warumi anamuogopa yeye[Mtume[S.A.W]."
Abu Sufyan aliongezea,"Wallahi,nikawa na uhakika na uhakika kwamba dini hii itaibuka mshindi mpaka mwishowe nikasilimu".[Bukhari #2782].
******* NA ALLAH NDIE MJUZI ZAIDI ******************

No comments:

Post a Comment