Kuna mambo ni ya lazima katika demokrasia,
ukiyakosa hayo demokrasia hakuna.
La kwanza
ni kwamba kila mtu lazima aweze kusema hisia zake kwa uhuru kabisa,
na maneno ya kila mtu lazima yasikilizwe. Hata kama mawazo ya mtu huyu hayapendwi kiasi gani,
au walio wengi wanamdhania anapotoka kiasi gani, siki tu. Kama mtu anapendwa kwa wema
wake, au hapendwi kwa visa vyake, hayo yote si kitu. Kila mtanzania, kila mtu kijijini,
kila mjumbe wa Halmashauri ya wilaya, kila mbunge, n.k.,
lazima aweze kusema kwa uhuru bila hofu ya vitisho, iwe katik amkutano iwe nje ya mkutano.
Watu wenye mawazo tofauti hata wakiwa wachache,
lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika majadiliano bila hofu ya kusumbuliwa,
mawazo yao yaje kushindwa katika hoja za majadiliano, siyo yashindwe kwa vitisho au
mabavu.Majadiliano yenyewe yatakayoleta uamuzi lazima yawape nafasi watu kusema kwa uhuru kabisa.
Na hata baada ya kuamua jambo watu wawe na uhuru kuendelea kulizungumzia jambo hilo. Maana
wale wachache wenye mawazo tofauti lazima wafahamu kuwa kama wanayo mawazo yenye maana,
na kama wakiyaeleza mawazo hayo vizuri, wanaweza kubadili mawazo ya wale
wengine walio wengi. Kadhalika wale
walio wengi lazima wawe tayari kuyashikilia mawazo yao mpaka wale
wachache waridhike kuwa uamuzi uliofanywa juu ya jambo hilo ulikuwa sawa.
Majadiliano lazima yaruhusiwe kuendelea, kwa uhuru kabisa. NA HIYO NI SEHEMU YA MAANA
YA UHURU WA MTU BINAFSI.
No comments:
Post a Comment