YAHITAJI AKILI YENYE
UTAMBUZI WA KINA KUNG'AMUA
VINGINEVYO UTAIONA NDEFU, AU HUTOELEWA KABISA...MUHIMU NI KUWA ASIYEJUA
MAANA HAAMBIWI
Nilikuta kitabu ndani kwangu, kilikua kitabu kikuu kuu sana. Kimeshiba
vumbi la kutosha tu, kana kwamba hakikuwa na mwenyewe. Nilistaajabu
nimeshindwaje kukiona kitabu hicho toka nilipoanza kuishi humo ndani.
Kitabu hicho kilikua na hadithi nyingi fupi fupi, lakini ni hadithi moja
tu iliyonitia wahka wa kutaka kuisoma. Ilianza kama ifuatavyo.
Hukooo ulimwenguni! palitokea Wapishi wakuu kutoka meko tofauti,
walikutana wakakubaliana kupika pishi la pamoja. Pishi ambalo lingeweza
kuliwa na walaji kutoka kila meko hadi milele. Pishi likapikwa,
lilipokuwa tayari likawekwa mezani tayari kwa kuliwa. Walaji walikuwa ni
wachache tu, lakini waliongezeka kadri siku zilivyozidi kwenda.
Walaji walifakamia Pishi hilo lililokuwa na vitamini nyingi kama mbwa
mwitu wavamiavyo lindo lao. Miaka mingi iliteketea, Pishi halikuchacha
na wala halikuisha. Kadri walivyokuwa wakila pishi hilo ndipo baadhi yao
walipopata kubaini dosari mbali mbali za pishi hilo kama vile, chumvi
kupungua, iliki kuzidi, ladha ya ndimu kutokuwepo, mafuta kuwa mengi mno
na kadhaalika. Walaji wengine walijonea sawa tu. Walipiga tonge za
ujazo na uzito tofauti tofauti. “Haya ndo maisha” walisikika.
Pamoja na dosari hizo hapakutokea mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzisema,
nafikiri kutokana na woga ama heshima kwa wapishi wao wakuu. Walaji
walinung’unika lakini mwisho wa siku kila mmoja alisikika akisema kuwa
hakupata kula Pishi tamu lenye ladha ya kipekee kama hilo katika umri
wake wote.
Paliwahi kutokea walaji waliodiriki kusema sema dosari hizo wazi wazi,
wengine walidiriki hata kusema hawataki kuendelea kula. Haikujulikana
walipotelea wapi. Ikatokea siku ambapo Wapishi wakuu walihama katika
ulimwengu huo na kwenda ulimwengu mwingine, kila Mpishi alihama kwa muda
wake. Bila shaka waliitwa kwenda kupika pishi kama hilo katika
ulimwengu mwengine wa mbli zaidi kwani waliondoka bila kuaga.
Pishi waliloliacha liliendelea kuwepo, pamoja na dosari zilizopata
kumulikwa na walaji Pishi hilo halikuisha. Miaka iliyoyoma kwa kasi.
Manung’uniko ya walaji yalipata nguvu na kasi kama jiwe lililoachiwa
kutoka mlimani. Walaji wengine hawakusita kudhihirisha kwa wenzao utamu
waliouhisi ambao waliona unazidi kuongezeka katika Pishi hilo, pamoja na
yote bado walionekana kama ni luba walioishiwa gundi na badala yake
wanatafuta nta ambayo hata ikipatikana haizidi ukali wa ile gundi yao ya
asili.
Ilifika wakati Ikaonwa ni bora walaji wote wakusanyane pamoja ili kila
mmoja asikike anatakaje juu ya Pishi hilo kongwe. Walaji wakakusanyika.
Sasa kila mmoja alikua huru kufyatua kauli na mawazo yake. Palizungumzwa
hapo mambo tele kwa tele. Pakawa mchana pakawa usiku. Siku zikasukana
na kuwa msitu. Ilifika kipindi Walaji walikosa staha sasa ikawa ni kama
vita vya wajuzi wa kutengeneza maneno yaliyo uchi.
Wapo waliosikika wakisema “Pishi limetushinda.. haliliki tena” wengine
waliropoka tu “tulimwage” wengine walidai “tulirudishe jikoni tukalipike
upya”, wengine wakadandia “mbona mama yako la kwake lilimshinda pia”
“Kama limekushinda, usishindane nalo liwache” mara wengine “Pishi
linahitaji mboga..kavu kavu haliliki” “wengine kavu hatujazowea” na hata
wapo waliodiriki kusema Wapishi walikosea kulipika Pishi hili kwa
pamoja, badala yake walipaswa kulipika kila mmoja sufuria lake na kisha
lingetafutwa sufuria jingine lenye mdomo mkubwa kuliko yote ambalo
lingechanganya mapishi yote mawili, basi ilimradi walaji wote walitoa
mapendekezo na madai yao.
Mimi kama msomaji nilitamani sana kuona walaji hao wangeishia wapi, kwa
bahati mbaya kile kitabu kilikua kimechanwa karatasi moja iliyobeba
kurasa mbili, kurasa ambazo nina hakika zilikua zimelenga kukata kiu ya
msomaji, kiu ya kutaka kujua ni nini kingejiri baina ya walaji hao dhidi
ya Pishi lile. Karatasi iliyobakia ilikuwa na ukurasa mmoja wa mwisho
ambao ulibeba sentsi moja tu ya mkiani mwa hadithi hiyo. Sentensi hiyo
iliishia kwa kusomeka “.............na hiyo ndiyo ikawa hatima ya Pishi
hilo lililopikwa takribani miaka hamsini iliyopita”.
No comments:
Post a Comment